Masuala Ibuka Yanayowasilishwa katika Vikatuni vya Ubongo Kids
Date
2025-11-11
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
East African Journal of Swahili Studies
Abstract
Utafiti huu ulilenga kujadili masuala ibuka kwenye vikatuni vya Ubongo Kids.
Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Elimu Burudani ambayo iliwekewa
msingi na Miguel Sabido (2003). Elimu Burudani ni nadharia iliyofumwa
kuelimisha na kubadilisha mitazamo ya jamii kupitia burudani. Nadharia ya
Elimu Burudani ilimsaidia mtafiti kuelewa jinsi vikatuni vya Ubongo Kids
vinavyoelezea hali halisi kuhusu maisha ya watu na jinsi watazamaji wanaweza
kuchochewa kujenga maana fulani kwa kulinganisha matukio katika kipindi na
maisha yao. Sampuli ya utafiti ilipatikana kwa kutumia mbinu ya usampulishaji
kimaksudi. Mbinu ya usampulishaji kimaksudi ilimhitaji mtafiti kuamua kwa
hiari yake sampuli iliyoweza kumpa data kutoka kwa video inayohusiana na
lengo la utafiti. Ukusanyaji wa data ulitumia mbinu ya kiwango kifu ambapo
hakuna masuala au maarifa mapya yaliyobainika na data ilianza kujirudia,
jambo linaloashiria kuwa ukubwa wa sampuli uliokusudiwa umefikiwa. Hivyo,
mtafiti aliteua video 10. Uteuzi wa video ulizingatia masuala ibuka, ubora wa
elimu kupitia burudani, na uhusiano wa moja kwa moja na malengo ya utafiti.
Pia, video zilichaguliwa kulingana na ubora wa kiufundi na kipindi cha ubunifu
kati ya mwaka wa 2014 na 2025. Data ilikusanywa kwa kutazama kauli na
matendo yaliyoashiria masuala ibuka na kauli yao kunukuliwa. Uchanganuzi
pamoja na uwasilishaji wa data ulifanyika kwa njia ya maelezo. Utafiti ulibaini
kuwa masuala ibuka katika vikatuui vya Ubongo Kids huwasilishwa kwa njia
rahisi kueleweka, yakilenga kuelimisha watoto kuhusu changamoto za sasa
kama mabadiliko ya tabianchi, ulinzi wa watoto, matumizi salama ya
teknolojia, umuhimu wa lishe bora, elimu na usafi wa mazingira. Matokeo ya
utafiti yatawafaidi walimu, wakuza mitalaa na watafiti wengine kwa kuonyesha
ufaafu wa vipindi vya watoto kama kiungo muhimu cha elimu kando na
kuburudisha.
Description
Keywords
Vikatuni, Ubongo Kids, Masuala ibuka, Elimu ya kidijitali, Uendelevu wa mazingira
Citation
Opondo, S. O., Kanyua, M. & Ntiba, O. (2025). Masuala Ibuka Yanayowasilishwa katika Vikatuni vya Ubongo Kids. East African Journal of Swahili Studies, 8(3), 15-32. https://doi.org/10.37284/jammk.8.3.3948
