Chuka University Digital Repository

Chuka University Repository is a Digital Hub for Knowledge Output From Chuka University.

Photo by @inspiredimages
 

Recent Submissions

Item
Suala la Ardhi katika Riwaya Teule za Kiswahili: Tathmini ya Kovu Moyoni na Kufa Kuzikana
(Chuka University, 2018) Njeru, Mary Kanyua
Ardhi ni mojawapo ya rasilimali muhimu katika maisha ya mwanadamu. Suala la rasilimali ya ardhi ulimwenguni hasa nchini Kenya limekuwa nyeti na kuibua mijadala ya kijamii na kiakademia tangu enzi za ukoloni na hata baada ya uhuru. Utafiti huu ulikusudia kuchunguza jinsi suala la ardhi limesawiriwa na waandishi wa riwaya teule za Kiswahili. Riwaya zilizohakikiwa ni Kufa Kuzikana (Walibora, 2003) na Kovu Moyoni (Habwe, 2014). Msisitizo ulikuwa kuangazia jinsi wasanii wa riwaya hizi walivyoangazia migogoro kuhusu ardhi kuonyesha matatizo yaliyotokana na mikinzano kuhusu rasilimali hiyo pamoja na athari zake. Hii ni kwa msingi kuwa fasihi ni mojawapo ya nyenzo inayoweza kuchangia kuangazia matatizo yanayokumba jamii yoyote iwayo. Aidha, ni chombo muhimu cha kuelimisha, kuhamasisha na kuzindua jamii pana kuhusu matatizo yake. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza jinsi Walibora na Habwe wametumia fasihi kudhihirisha mizozo ya ardhi kwa kurejelea tungo zao, kuchunguza jinsi ambavyo walitumia fani za lugha kuwasilisha athari za mizozo ya ardhi na kubainisha suluhisho walilolitoa kama wasanii walio katika sehemu ya jamii zilizokumbwa na migogoro ya ardhi. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Baadaukoloni ambayo inahusishwa na kazi za Cesaire (1950), Fanon (1961) Said (1978) na Bhabha (1994), ambayo ilitumika ili kufafanua jinsi waandishi wa riwaya teule wamedhihirisha athari za ukoloni katika suala la ardhi. Utafiti huu ulitumia uteuzi wa sampuli wa kimakusudi kama njia ya kutathmini riwaya teule. Data ilipatikana kutoka kwenye matini iliyoteuliwa kimakusudi. Mtafiti alisoma riwaya husika kwa kina na kubaini maneno na mafungu ya maneno yaliyohusiana na suala la ardhi. Aidha, mtafiti alihakiki na kuchunguza jinsi wasanii wa riwaya za Kufa Kuzikana na Kovu Moyoni wamefafanua matatizo ya ardhi pamoja na suluhisho wanazotoa. Uchanganuzi wa kimaelezo wa data ulifanywa na kuwasilishwa kwa maandishi ya kinadhari. Ilibainika kuwa wasanii wa riwaya teule wamerejelea suala la ardhi nchini Kenya kama tatizo la jamii ambamo riwaya hizo ziliibuka huku wakiwasawiri Wakenya kama wahusika katika kazi zao kwa mujibu wa vipindi mbalimbali vya kihistoria. Vilevile, wameangazia mambo mbalimbali ambayo yanaweza kutumika ili kusuluhisha matatizo ya ardhi nchini. Utafiti huu utawanufaisha wahakiki wa fasihi katika kushadidia mtazamo kwamba, fasihi inaakisi kikamilifu matatizo yanayoibuka katika jamii ilimoibuka. Kwa hivyo, ni chombo madhubuti kinachoweza kutumiwa kutatua matatizo hayo.
Item
Usawiri wa Motifu za Kimazingira katika Tamthilia Teule za Said Ahmed Mohamed na Timothy Arege: Uhakiki wa Kiekolojia
(Chuka University, 2022) Njeru, Mary Kanyua
Suala la mabadiliko ya tabianchi limeibua mijadala katika viwango vya kitaifa na kimataifa. Kwa msingi huu, kazi mbalimbali za kifasihi zimebuniwa kwa kuangazia uharibifu wa mazingira asilia, athari zake na mwito wa kuhifadhi mazingira. Utafiti huu ulikusudia kuchunguza motifu za kimazingira zinazojitokeza katika tamthilia teule za Said Ahmed Mohamed na Timothy Arege. Msisitizo ulikuwa kuangazia jinsi wasanii wa matini hizi wamesawiri uharibifu wa mazingira, kuonyesha matatizo yanayotokana na uharibifu huo pamoja na athari zake. Hii ni kwa sababu fasihi huwasilisha hali, maingiliano na mikinzano miongoni mwa binadamu na mazingira. Hivyo, ni mojawapo ya nyenzo inayoweza kuchangia katika kuangazia matatizo yanayokumba jamii yoyote ile. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza jinsi motifu za kimazingira zilivyosawiriwa katika tamthilia teule za Said Ahmed Mohamed na Timothy Arege, kujadili jinsi mtindo ulivyotumika kusawiri motifu za kimazingira katika tamthilia teule na hatimaye kutathmini mchango wa motifu za kimazingira katika uhifadhi wa mazingira kwa mujibu wa tamthilia teule. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya uhakiki wa kiekolojia iliyoasisiwa na Glotferty (1996). Nadharia hii hujikita katika uchambuzi wa kazi za kifasihi kwa kuonyesha uhusiano na utegemeano baina ya binadamu na mazingira. Utafiti huu ulifanyiwa maktabani ambapo uteuzi wa sampuli wa kimakusudi ulitumiwa kuteua matini teule. Data ya utafiti ilikusanywa kupitia usomaji wa kina wa matini teule, ikapangwa kwa mujibu wa madhumuni ya utafiti na kuchanganuliwa kwa kuzingatia mihimili ya nadharia ya uhakiki wa kiekolojia. Baadaye, data ilifasiriwa kwa kutumia mbinu elezi. Matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha kuwa tamthilia teule za Kiswahili zilizochunguzwa zimeangazia masuala mbalimbali ya kimazingira pakiwemo chanzo cha uharibifu wa mazingira, athari za uharibifu huo pamoja na kubainisha njia ambazo zinaweza kutumika katika uhifadhi wa mazingira. Utafiti huu unatarajiwa kuwa na manufaa kwa wasomi na wahakiki wa fasihi kwa kuangazia suala la motifu za kimazingira kwa mkabala wa uhakiki wa kiekolojia. Vilevile, umetoa mchango katika uwanja wa fasihi mazingira kwa kuongezea suala la motifu za kimazingira. Isitoshe, utafiti huu ni muhimu kwa washikadau wote wa masuala ya kimazingira Barani Afrika na ulimwengu kwa jumla.
Item
Koja la Taaluma za Insia
(Karljamer Publishers Limited, 2019) Athumani Salum Ponera & Zuhura A. Badru ( Wahariri)
Utangulizi Ardhi ni mojawapo ya rasilimali muhimu katika maisha ya mwanadamu. Suala la ardhi ulimwenguni, na hasa nchini Kenya, limekuwa nyeti na kuibua mijadala ya kijamii na kiakademia tangu enzi za ukoloni. Vita vya ukombozi dhidi ya utawala dhalimu wa ukoloni katika mataifa mengi barani Afrika vilichochewa na msukumo wa utwaaji wa ardhi kutoka kwa wakoloni. Fasihi ni mojawapo ya nyenzo inayoweza kuchangia katika kuangazia matatizo yanayoikumba jamii yoyote iwayo. Kazi hii inachunguza jinsi ambavyo suala la mizozo ya ardhi limesawiriwa katika riwaya ya Kiswahili kwa kurejelea riwaya ya Kufa Kuzikana (Walibora, 2003). Mjadala unaongozwa na nadharia ya Baadaukoloni ambayo inahusishwa na kazi za Cesaire (1950), Fanon (1961), Said (1978) na Bhabha (1994). Aidha, tunafafanua jinsi riwaya ya Kiswahili inavyodhihirisha athari za ukoloni katika suala la mizozo ya ardhi pamoja na kuonesha msingi ambao jamii ya Kenya imejengeka kuhusu athari zinazotokana na umiliki wa ardhi. Mjadala unafanywa kwa kutumia misingi ya nadharia ya baadaukoloni.
Item
Fasihi na Masuala Ibuka: Kwa Heshima ya Marehemu Prof. Ken Walibora
(RealText Publishers, 2025) Mosol Kandagor, John Kobia, Iribe Mwangi, Leonard Chacha Mwita, and Fred Simiyu Wanjala (Wahariri)
Kuwepo kwa mshikamano wa kitaifa husaidia katika kukuza ushirikiano wa kimaadili na kuandaa nafasi za kimaisha kwa kila mtu katika taifa lolote lile. Nchini Kenya, kumekuwa na mizozo mingi kwa misingi ya kikabila ambayo kwa muda mrefu imetishia kuvuruga mshikamano wa kitaifa. Fasihi ni chombo ambacho kinaweza kutumiwa kujenga msingi wa utu, usawa, upendo na usalama wa watu katika jamii. Makala hii inakusudia kuangazia jinsi ambavyo mwandishi Ken Walibora amesawiri mshikamano wa kitaifa, kuonyesha chanzo cha mizozo katika jamii, juhudi za kuleta mshikamano na changamoto za kuleta mshikamano huo. Makala hii itaongozwa na nadharia ya uhalisia iliyoasisiwa katika Karne ya 19 na E. Goffman. Kwa mjibu wa nadharia hii, mwandishi husukumwa na nia ya kuusawiri uhalisia katika ukamilifu na wakati wake maalum. Riwaya ya Kufa Kuzikana (Walibora, 2003) iliteuliwa kimakusudi kwa kuwa maudhui yake makuu yanahusiana moja kwa moja na mada ya makala hii. Kazi hii ni muhimu katika kuthibitisha kuwa fasihi ya Kiswahili inatekeleza dhima muhimu katika kuhamasisha jamii kuhusu haja ya kuwepo kwa mshikamano wa kitaifa.
Item
Usawiri wa Motifu za Kimazingira Katika Tamthilia ya Kiswahili: Tathmini ya Majira ya Utasa (Arege, 2015)
(East African Nature & Science Organization (EANSO), 2022-06-10) Njeru, Mary K.; Kobia, John M.; Musyimi, Dorcas M.