Ubabedume katika tamthilia ya bembea ya maisha (2022)

Abstract

Mfumo-dume humpa thamani kubwa mwanamume huku ukimdhalilisha mwanamke kwa sababu ya jinsia yake. Imani hii dunishi imo katika itikadi na tamaduni zinazohimiliwa na mfumo wa muundo wa kijamii ambao mwanamume anapewa nguvu na uwezo zaidi dhidi ya mwanamke katika nyanja zote za maisha hususan kiutawala, kiuchumi, kidini, kisiasa na kijamii. Basi, makala hii ililenga kuchunguza jinsi mwandishi wa tamthilia ya Bembea ya Maisha (2022) alivyomsawiri mhusika wa jinsia ya kiume katika kazi yake ili kuweka wazi shughuli za ubabedume zilizojengwa katika mila, itikadi na utamaduni wa jamii husika. Data ya makala ilipatikana kwa kuisoma tamthilia teule kisha kuichanganua kwa kutumia Nadharia ya Ubabedume ambayo hulenga kubainisha nguvu na mamlaka yanayomilikiwa na jinsia ya kiume, hasa kutokana na utamaduni wa jamii husika. Matokeo ya utafiti yalibainisha kuwa mhusika wa jinsia ya kiume amesawiriwa kama mtegemezi, mrithi wa mali, ameruhusiwa kupata mtoto nje ya ndoa, haruhusiwi kujishughulisha na kazi za nyumbani, anaitwa gumba kwa kutopata watoto na anayejitwika majukumu yote ya nyumbani. Masuala haya yamekithiri katika jamii za leo. Ikiwa nchi zinazoendelea zitapiga hatua katika maendeleo, basi usawa wa kijinsia unahitaji kutiliwa maanani na jamii zote. Istilahi Muhimu: Usawiri, Mfumo-dume, Taswira, Ubabedume, Jinsia

Description

Keywords

Citation

Musyimi D. M. and Nyagah S. K.(2023) Ubabedume katika tamthilia ya bembea ya maisha In: Isutsa, D. K. (Ed.). Proceedings of the Chuka University 8th Annual International Research Conference held in Chuka University, Chuka, Kenya from 24th to 25th November, 2022. 218-223 pp.