Usawiri wa motifu za kimazingira katika tamthilia teule za Said Ahmed Mohamed na Timothy Arege: Uhakiki wa kiekolojia

Thumbnail Image

Date

2022

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

Chuka University

Abstract

Suala la mabadiliko ya tabianchi limeibua mijadala katika viwango vya kitaifa na kimataifa. Kwa msingi huu, kazi mbalimbali za kifasihi zimebuniwa kwa kuangazia uharibifu wa mazingira asilia, athari zake na mwito wa kuhifadhi mazingira. Utafiti huu ulikusudia kuchunguza motifu za kimazingira zinazojitokeza katika tamthilia teule za Said Ahmed Mohamed na Timothy Arege. Msisitizo ulikuwa kuangazia jinsi wasanii wa matini hizi wamesawiri uharibifu wa mazingira, kuonyesha matatizo yanayotokana na uharibifu huo pamoja na athari zake. Hii ni kwa sababu fasihi huwasilisha hali, maingiliano na mikinzano miongoni mwa binadamu na mazingira. Hivyo, ni mojawapo ya nyenzo inayoweza kuchangia katika kuangazia matatizo yanayokumba jamii yoyote ile. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza jinsi motifu za kimazingira zilivyosawiriwa katika tamthilia teule za Said Ahmed Mohamed na Timothy Arege, kujadili jinsi mtindo ulivyotumika kusawiri motifu za kimazingira katika tamthilia teule na hatimaye kutathmini mchango wa motifu za kimazingira katika uhifadhi wa mazingira kwa mujibu wa tamthilia teule. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya uhakiki wa kiekolojia iliyoasisiwa na Glotferty (1996). Nadharia hii hujikita katika uchambuzi wa kazi za kifasihi kwa kuonyesha uhusiano na utegemeano baina ya binadamu na mazingira. Utafiti huu ulifanyiwa maktabani ambapo uteuzi wa sampuli wa kimakusudi ulitumiwa kuteua matini teule. Data ya utafiti ilikusanywa kupitia usomaji wa kina wa matini teule, ikapangwa kwa mujibu wa madhumuni ya utafiti na kuchanganuliwa kwa kuzingatia mihimili ya nadharia ya uhakiki wa kiekolojia. Baadaye, data ilifasiriwa kwa kutumia mbinu elezi. Matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha kuwa tamthilia teule za Kiswahili zilizochunguzwa zimeangazia masuala mbalimbali ya kimazingira pakiwemo chanzo cha uharibifu wa mazingira, athari za uharibifu huo pamoja na kubainisha njia ambazo zinaweza kutumika katika uhifadhi wa mazingira. Utafiti huu unatarajiwa kuwa na manufaa kwa wasomi na wahakiki wa fasihi kwa kuangazia suala la motifu za kimazingira kwa mkabala wa uhakiki wa kiekolojia. Vilevile, umetoa mchango katika uwanja wa fasihi mazingira kwa kuongezea suala la motifu za kimazingira. Isitoshe, utafiti huu ni muhimu kwa washikadau wote wa masuala ya kimazingira Barani Afrika na ulimwengu kwa jumla.

Description

library@chuka.ac.ke www.chuka.ac.ke

Keywords

Mabadiliko ya tabianchi, Uharibifu wa mazingira, Motifu za kimazingira, Uhifadhi wa mazingira, Tamthilia ya Kiswahili, Said Ahmed Mohamed, Timothy Arege, Fasihi ya mazingira, Uhakiki wa kiekolojia, Fasihi na mazingira, Athari za mazingira, Mtindo wa kifasihi, Masuala ya kimazingira, Uhusiano wa binadamu na mazingira, Fasihi ya Kiswahili ya kisasa

Citation