Mwendelezo wa tamthilia ya mashetani (1971) katika mashetani wamerudi (2016): uhakiki wa kimwingilianomatini
Loading...
Date
2024
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Chuka University
Abstract
Utafiti huu ulichunguza mwendelezo wa tamthilia ya Mashetani (1971) katika Mashetani Wamerudi (2016). Malengo ya utafiti huu yalikuwa: kuchunguza mwendelezo wa maudhui ya tamthilia ya Mashetani (Hussien, 1971) katika Mashetani Wamerudi (Mohamed, 2016), Kutathimini athari za mwendelezo wa mtindo katika Mashetani kwenye Mashetani Wamerudi na kubainisha viwango vya mwingilianomatini katika tamthilia za Mashetani na Mashetani Wamerudi. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Mwingilianomatini iliyoasisiwa na Julia Kristeva (1986). Mwingilianomatini ni dhana inayoonyesha kutegemeana, kuhusiana na kuathiriana kwa matini. Hii ina maana kuwa kazi za fasihi hurejelea na kuendeleza kazi tangulizi. Kulingana na Kristeva kazi ya fasihi huonyesha kuathiriana na matini nyingine, huzigeuza na kuziendeleza kwa ubunifu. Mihimili iliyoongoza utafiti huu ni pamoja na: matini yoyote ile ni madadiliko ya mpangilio wa matini nyingine, kazi za fasihi huundwa kutokana na mifumo ya kanuni na tamaduni mbalimbali zilizowekwa na kazi tangulizi. Matini za fasihi huchota, kunukuu na kuiga kazi nyingine. Data ya utafiti ilipatikana maktbani kutokana na usomaji na uchambuzi wa matini teule. Sampuli ya kimaksudi ilitumika kuteua tamthilia za Mashetani na Mashetani Wamerudi kwa sababu matini hizi zinadhihirisha mwingiliano wa aina fulani. Vipengele vinavyodhihirisha mwingilianomatini vilibainishwa na kuchanganuliwa ili kuonyesha mwendelezo wa kimatini uliopo. Utafiti huu umedhihirisha kwamba kuna mwendelezo wa tamthilia ya Mashetani katika Mashetani Wamerudi. Imebainika kwamba mwandishi wa tamthilia ya Mashetani Wamerudi ameiga, amerejelea na kuendeleza tamthilia ya Mashetani katika kiwango cha maudhui, mtindo na viwango vya kimwingilianomatini. Matokeo ya utafiti huu yaliashiria kuwa kuna mwendelezo wa maudhui ya Ukoloni mamboleo, elimu ya kibwege, utabaka na ufisadi ni baadhi ya masual makuu amabyo yanajitokeza katika tamthilia ya Mashetani Wamerudi. Katika lengo la pili utafiti umethibitisha kuwa Said Mohamed amerejelea na kuiga mtindo wa kiutunzi wa mtangulizi wake. Matumizi ya mtindo wa usimulizi, nyimbo, majigambo, ushairi na maigizo ni baadhi ya vipengele vya kiutunzi ambavyo vimetumika kama malighafi ya kiutunzi katika kazi ya Said Mohamed. Hatimaye, utafiti huu ulibainisha kuwa kuna urejelezi wa moja kwa moja wa tamthilia ya Mashetani kupitia njia zifuatazo: Urejelezi wa matini za Kihistoria, urejelezi wa kiutohozi pamoja na uigaji. Matokeo ya utafiti huu yataweka msingi kwa waandishi na walimu wa fasihi katika kuonyesha jinsi fasihi inavyoingiliana kwa kurejelea vipindi tofauti vya kihistoria na kiutamanduni.
Description
Tasnifu iliyowasilshwa katika Shule ya Mafuzu ili kutosheleza baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Chuka
wasimamizi: Dkt Allan Mugambi,Dkt Dorcas Musyimi
Keywords
Kimwingilianomatini, Mwendelezo wa kimatini, Tamthilia ya Kiswahili, Maudhui ya kifasihi, Mtindo wa kiutunzi, Urejelezi wa matini, Fasihi linganishi.
Citation
Mutuma, K. M. (2024). Mwendelezo wa tamthilia ya Mashetani (1971) katika Mashetani Wamerudi (2016): Uhakiki wa kimwingilianomatini (Master’s thesis, Chuka University).
