Browsing by Author "Mwilaria Reuben"
Now showing 1 - 1 of 1
- Results Per Page
- Sort Options
Item Sitiari za kiafya katika matini teule za fasihi ya kiswahili ya watoto(Chuka University, 2024) Mwilaria ReubenHaja ya kuimarisha viwango vya afya ulimwenguni imechangia kujumuishwa kwa taaluma mbalimbali kama vile fasihi katika vita dhidi ya changamoto za kiafya. Kazi mbalimbali za kifasihi zimebuniwa zikiangazia masuala ya kiafya yanayoathiri jamii na namna ya kuyasuluhisha. Utafiti huu ulijikita katika utanzu wa fasihi ya Kiswahili ya Watoto kwa lengo la kuchanganua sitiari za kiafya katika matini teule za fasihi ya Kiswahili ya Watoto. Uliongozwa na malengo yafuatayo: Kujadili aina za sitiari za kiafya katika vitabu teule vya fasihi ya Kiswahili ya Watoto, kuchunguza mtindo uliotumika kuwasilisha sitiari za kiafya katika vitabu teule na kufafanua masuala mtambuko yaliyowasilishwa na sitiari za kiafya katika vitabu teule vya fasihi ya Kiswahili ya Watoto. Vitabu viteule ni: Siku ya Ukimwi (Kobia, 2008), Pendo katika Shari (Momanyi, 2008), Sitaki Iwe Siri (Matundura, 2008), Madhila ya Bi. Shufaa (Bakari, 2008), Kosa la Marehemu (Panja, 2010) na Nimefufuka (Nandwa, 2011) katika msururu wa “Afya Yangu.” Vitabu hivi vilichaguliwa kimakusudi kwa sababu ya upekee wake katika kuangazia suala la afya, ambalo ni muhimu katika jamii na huchangia katika kuafikiwa kwa maendeleo endelevu. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia Changanuzi ya Sitiari ya Dhana ya Johnson na Lakoff (1980) na nadharia ya Umitindo ya Leech (1969). Nadharia Changanuzi ya Sitiari ya Dhana ilitumika kujadili aina za sitiari za kiafya na kufafanua masuala mtambuko yaliyowasilishwa na sitiari za kiafya katika vitabu teule. Nadharia ya umitindo ilitumika kuchunguza mtindo uliotumika kuwasilisha sitiari za kiafya katika vitabu teule. Utafiti huu ulifanyiwa maktabani. Data ilipatikana kwa kusoma vitabu teule kwa kina na kunakili maneno ya kisitiari, vishazi na sentensi zilizorejelea masuala ya kiafya. Data hiyo ilikusanywa na kupangwa kulingana na malengo ya utafiti. Ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya maelezo. Matokeo ya utafiti huu ni kuwa ulibainisha aina mbalimbali za sitiari za kiafya. Pia, iligunduliwa kuwa fasihi ya Kiswahili ya Watoto ilifaa kutumiwa kama njia mbadala ya kuelimisha jamii kuhusu athari za masuala mtambuko kama vile afya, dawa za kulevya na masuala ya kijnsia yanayoathiri afya katika jamii kwa sababu iliweza kusomwa na watu wa viwango mbalimbali vya elimu. Utafiti huu pia ulibainisha na kupanua mawanda ya matumizi ya sitiari na fasihi ya Kiswahili ya Watoto katika kuboresha changamoto za kiafya na kuwa marejeleo ya tafiti za baadaye. Utafiti huu ulipendekeza kuwa, washikadau katika sekta ya afya wajumuishe fasihi ya Kiswahili ya Watoto katika kufunza masuala ya kiafya. Pia, lugha ya kisitiari itumiwe katika kuangazia masuala ya kiafya katika jamii ambazo masuala hayo hayatajwi hadharani kwa sababu ya tamaduni hasi. Pia, kulikuwa na haja ya jamii kuharamisha matumizi ya dawa za kulevya na ubagusi wa kijinsia. Waliofaidika na utafiti huu ni washikadau wanaofunza jamii kuhusu umuhimu wa afya bora, madhara ya dawa za kulevya na masuala ya kijinsia yanayosababisha afya duni.
