Muundo wa Sentensi ya Kiigembe: Mtazamo wa Eksibaa
Abstract
Sintaksia ni taaluma inayojihusisha na uchambuzi wa miundo ya sentensi. Utafiti huu ulichanganua muundo wa sentensi ya Kîîgembe katika taaluma ya sintaksia. Kati ya vipashio vinavyotumika katika taaluma ya kisintaksia ni kama vile, kirai na kishazi ambavyo ndivyo vijenzi vya sentensi. Kîîgembe huzungumzwa katika maeneo ya kiutawala ya Igembe ya Kati, Igembe Kaskazini na Igembe Kusini katika Kaunti ya Meru, Kenya. Mwauo wa Maandishi ulibainisha kuwa, hakuna utafiti uliofanywa kuhusu muundo wa sentensi ya Kîîgembe kwa mtazamo wa Eksibaa. Malengo ya utafiti huu yalikuwa; kueleza miundo ya virai na kufafanua miundo ya vishazi vya sentensi ya Kîîgembe kwa mujibu wa Nadharia ya Eksibaa. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Eksibaa iliyoasisiwa na Chomsky. Nadharia hii hubainisha virai na kuonyesha mpangilio wa viambajengo mbalimbali katika kategoria ya sintaksia. Kwa hivyo, nadharia hii ilifaa utafiti huu kwa kufafanua aina za virai na mpangilio wa kategoria za viambajengo mbalimbali katika sentensi ya Kîîgembe. Katika Nadharia ya Eksibaa, kirai ni kipashio cha muundo chenye neno moja au zaidi lakini kisicho na muundo wa kikundi nomino na kikundi tenzi. Kwa hivyo, ilifaa katika kueleza vipashio vya sentensi ya Kîîgembe na kuchanganua muundo wake. Data ya utafiti huu ilikuwa sentensi za Kîîgembe ambazo mtafiti alizipata nyanjani na pia mtafiti kuzalisha mwenyewe kutokana na umilisi wake kama mzawa wa lahaja hii. Utafiti huu ulibainisha miundo tofauti ya sentensi za Kîîgembe na kubainisha sheria zinazotawala uunganishwaji wa vipashio vinavyojaliza sentensi ya Kîîgembe. Data ya utafiti huu ilikuwa sentensi za Kîîgembe mia na ishirini zilizotumika katika uchanganuzi wa utafiti huu, sentensi hizo zilijumuisha; sentensi sahili, sentensi ambatano na sentensi changamano. Kwa hivyo, kila aina ya sentensi ilichanganuliwa kwa sentensi arubaini. Katika awamu ya uchanganuzi wa data, utafiti huu ulichanganua miundo ya virai kama vile; virai nomino, virai vielezi, virai vivumishi, virai tenzi na virai vihusishi huku ikibainika kuwa kulingana na Nadharia ya Eksibaa, sentensi ya Kîîgembe ina miundo anuai ya virai vyake. Aidha, utafiti huu ulichanganua aina za vishazi kama vile vishazi tegemezi ambavyo huwakilishwa na vitambulisho vifuatavyo; nkîthîrwa, nûntû bwa, rîrîa, kinya kwethîrwa, nî kenda na kethîrwa. Vishazi huru na vishazi viambatani vimefafanuliwa miundo yake pia na kuonyesha jinsi kichwa humiliki viambajengo vingine ili kuunda sentensi mbalimbali. Viambajengo hivi viliweza kuchanganuliwa kwa lengo la kufanikisha muundo wa sentensi ya Kîîgembe. Matokeo ya utafiti huu yalibainisha isimu miundo kwa kubainisha muundo wa sentensi ya Kîîgembe. Pia, utafiti huu unaweza kusaidia lugha za Kibantu kufanyiwa utafiti zaidi kwani lahaja ya Kîîgembe inaweza kutoa mwanga kuhusu lugha za Kibantu. Aidha, ulisaidia kuhifadhi Kîîgembe katika maandishi.